RAIS
Jakaya Kikwete amemteua Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba kuwa
Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Tanzania. Pia amemteua na
Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani kuwa makamu wake.
Akitangaza
Tume hiyo Ikulu, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema Tume hiyo
itasaidiwa na Sekretarieti itakayoogozwa na Katibu Mtendaji, Asaa Ahmad
Rashid na Naibu wake ni Casmir Sumba Kyuki.
Hii ni mara ya pili
kwa Warioba, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali ambaye pia aliwahi
kuwa Jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Mazingira kupewa jukumu la
kusimamia tume zinazovuta hisia za mamilioni ya Watanzania kwani ndiye
aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kuondoa Kero ya Rushwa nchini iliyoundwa
na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.
Jaji Ramadhani kwa
upande wake, mbali ya kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kwa miaka sita, wadhifa
aliokuwa nao hadi alipostaafu Desemba 27, 2010 na nafasi yake yake
kuchukuliwa na Jaji Mkuu wa sasa, Mohamed Chande Othman alikuwa, Makamu
Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na baadaye Tume ya
Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa wadhifa huo huo. Pia alikuwa Brigedia
Jenerali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), hadi alipostaafu mwaka
1997.
Kwa upande wa Asaa kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Mkuu
wa Wizara ya Sheria Zanzibar wakati Kyuki alikuwa Mwandishi Mkuu wa
Sheria katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Tanzania Bara.
Rais
Kikwete aliwaambia wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo
mbalimbali vya habari kwamba uteuzi wa Tume hiyo ni hatua ya kwanza
muhimu katika mchakato wa kuiwezesha nchi kupata Katiba Mpya ifikapo
mwaka 2014.
“Sheria yetu inaelekeza Tume hii iwe imekamilisha
kazi yake ndani ya miezi 18, sasa kama wakianza kazi tuseme Mei watakuwa
na miezi minane mwaka huu na kwa maana hiyo mwakani inabidi wamalize
kazi hiyo Oktoba, miezi 18 itakuwa imekamilika,”alisema Rais Kikwete na
kuongeza:
“Sasa kama ni hivyo mimi sioni kwa nini ifikapo mwaka 2014 tusiwe na Katiba Mpya… hili linawezekana kabisa.” Wajumbe wengine
Tume
hiyo ina uwakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii. Yumo
mwanadiplomasia wa siku nyingi Waziri Mkuu Mstaafu na Katibu Mkuu wa
uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Dk Salim Ahmed Salim,
Mshauri wa wa Chadema, Profesa Mwesiga Baregu na Mkuu wa Idara ya
Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Dk
Sengondo Mvungi.
Tume hiyo ambayo inaundwa na wajumbe 30 nusu
kutoka kila upande wa Muungano, pia inawajumuisha aliyewahi kuwa
Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Said El Maamry, Mbunge
wa Viti Maalumu, Al-Shaymaa Kwegyir, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu
Nyerere (MNF), Joseph Butiku na Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha
Dar es Salaam (UDSM), Profesa Palamagamba Kabudi.
Rais Kikwete
aliwataja wajumbe wengine wa Tume hiyo kutoka Tanzania Bara kuwa ni
Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Yahya Msulwa, Mwenyekiti
wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Esther Mkwizu, Riziki
Mngwali, Richard Lyimo, John Nkolo, Jesca Mkuchu, Humphrey Polepole,
Maria Kashonda na Mwantumu Malale.
Wajumbe kutoka Zanzibar ni
wamo Mwandishi wa habari mkongwe, Ally Salehe, Fatma Said Ali, Omar
Sheha Mussa, Raya Salim Hamadi, Awadh Ali Said, Ussi Khamis Haji, Salma
Maoulidi, Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohammed Mshamba, Kibibi Mwinyi
Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed na Abubakar Mohammed Ali.
Rais
Kikwete alisema mchakato wa uteuzi wa wajumbe hao ulizingatia matakwa
ya kisheria yanayomwelekeza kushauriana na Rais wa Zanzibar.
Alisema
kabla ya kuteua majina hayo, walipokea mapendekezo ya majina zaidi ya
550 kutoka kwa wadau mbalimbali akisema ilikuwa kazi ngumu kuyachuja na
kubaki na majina hayo kama sheria inavyoelekeza.
“Tumejitahidi
kadri ya uwezo wetu maana kama si haya mapendekezo pengine tungeishia
kuteua wale tunaowafahamu tu, lakini tumejitahidi kugusa kila kundi.
Tunafahamu kwamba hatuwezi kumridhisha kila mtu, lakini wale ambao
hawakupata nafasi katika Tume basi watatumia fursa nyingine ambazo zipo
kupitia mchakato huu,” alisema Rais Kikwete.
Muda wa Tume Rais
Kikwete alisema wajumbe wa Tume hiyo wataapishwa wakati wowote kuanzia
sasa ili kuwawezesha kuanza safari yao ya miezi 18 ya kukusanya maoni ya
wananchi kuhusu Katiba Mpya na kukamilisha kuandikwa kwa Katiba hiyo.
Rais
alisema Tume hiyo baada ya kukamilisha kazi yake ya kukusanya maoni ya
Watanzania na kutengeneza rasimu ya Katiba, zitakuwa zimebaki hatua
mbili muhimu ambazo ni kuundwa kwa Bunge maalumu na kura ya maoni.
“Baada
ya hatua hiyo kukamilika, rasimu itawasilishwa katika Bunge maalumu
ambalo litaundwa kwa ajili ya kujadili na kuchambua mambo yanayofaa
yaliyomo katika rasimu hiyo, Bunge hili litakuwa kwa ajili hiyo tu na
likishakamilisha kazi yake basi muda wake utakuwa umeisha” alisema Rais
Kikwete.
Alisema baada ya mambo ya msingi kupitishwa na Bunge
hilo, mchakato huo utarejeshwa kwa wananchi ambao watapiga kura za maoni
kama wataona yaliyopitishwa yanafaa au la.
Rais ametangaza
kuundwa kwa Tume hiyo siku chache tangu yafanyike mabadiliko katika
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, katika Mkutano wa Sita wa Bunge la 10,
marekebisho ambayo yalizua manung’uniko kutoka kwa wabunge wa CCM.
Katika
hotuba yake ya Desemba 31, 2010, Rais Kikwete aliahidi kuanzisha
mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya ambayo alisema italivusha Taifa
katika miaka mingine 50 ikiimarisha udugu na mshikamano wa Watanzania.
Wateule wanena Wakizungumza
kwa nyakati tofauti, baadhi yawajumbe walioteuliwa katika Tume hiyo
walisema kuwa ni mapema mno kuzungumzia uteuzi wao.
Dk Mvungi
alisema kazi hiyo ni kubwa kwa kuwa wanaotumikiwa ni wananchi, huku
akiomba kupewa muda hadi leo ili aweze kutafakari cha kuzungumza.
“Muda
mfupi uliopita ndiyo nilipata taarifa ya uteuzi huo ila nahitaji
kujishauri kwanza pia kusikiliza ushauri wa familia yangu, naomba unipe
muda hadi kesho (leo), naweza kuwa na cha kuzungumza zaidi,” alisema Dk
Mvungi.
Kwa upande wake Butiku alisema mpaka alipokuwa akipigiwa
simu kuulizwa alivyopokea uteuzi wake alikuwa hajapata taarifa za uteuzi
huo. Alisema atazungumza mara baada ya kuthibitisha rasmi kuwa
ameteuliwa.
“Hivi tunavyozungumza ndiyo nafika Musoma nikitokea
Mwanza, sijapata taarifa yoyote, ngoja kwanza nisubiri taarifa rasmi ili
niweze kuzungumza vizuri.”
|