Tuesday, February 28, 2012

MAKAMBA NA ZITTO UMRI WA KUGOMBEA URAIS UWE 35,



MBUNGE wa Bumbuli (CCM), January Makamba na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe wametaka umri wa kugombea urais wa Tanzania uanzie miaka 35 badala ya 41 kama ilivyo sasa.

Wakizungumza kwenye Kongamano la Katiba na Vijana lililoandaliwa na Taasisi ya Femina HIP, Dar es Salaam jana, Zitto na Makamba pia walitaka umri wa kupiga kura uanzie miaka 16 badala ya 18.

Akichangia hoja, Makamba alisema ili kugombea urais katika nchi nyingi za Afrika Mashariki, raia husika anatakiwa kuwa na umri wa miaka 35.

“Hatutakuwa tumeanza sisi kwa sababu nchi nyingi duniani nafasi ya urais inagombewa kuanzia miaka 35, kwa hiyo vijana tuangalie suala hilo katika mchakato wa Katiba Mpya inayokuja,” alisema.

Makamba alisema Katiba Mpya inayokuja iwawezeshe vijana kupiga kura wakiwa na umri wa miaka 16 badala ya 18: “Umri wa kuanzia miaka 16 unatosha kabisa kuchanganua ni kiongozi wa aina gani anafaa kuchaguliwa.”

Kauli ya Makamba iliungwa mkono na Zitto ambaye alizitaja nchi za Kenya, Uganda na Burundi kuwa urais unagombewa kuanzia miaka 35.

“Hata sisi Tanzania wagombea wetu wanaweza kugombea wakiwa na umri wa miaka 35 kama zilivyo nchi za wenzetu ili kuwapa vijana nafasi za kuongoza nchi,” alisema na kuongeza kuwa anamwunga mkono Makamba katika suala hilo.

Zitto akichangia hoja, pia aliunga mkono umri wa kupiga kura kuwa miaka 16 akisema hiyo itawapa nafasi vijana wengi kushiriki katika kuchagua viongozi wao.

“Zamani umri wa kupiga kura ulikuwa miaka 21, ukashushwa ikawa miaka 18, kwa wakati tulionao sasa, uwezo wa vijana ni mkubwa, wanaweza kuchagua viongozi wakiwa na miaka 16,” alisema.

Hata hivyo, Zitto alitoa angalizo kwa vijana akisema katiba pekee haiwezi kuwaletea maendeleo... “Vijana wasisubiri Katiba Mpya kuwa ndilo litakuwa suluhisho la matatizo bali, itaweka mazingira rafiki kwa vijana wanaojishughulisha.”

Aliwataka vijana wa Tanzania wasikwepe kujadili Katiba Mpya na kuwachia wanasiasa kwani jukumu hilo ni la kwao pia.

“Wanasiasa muda mwingi wanajadili mambo yanayohusu maslahi yao kama vile muda wa kukaa madarakani lakini, mambo yanayowahusu vijana yatajadiliwa kwa ufanisi na vijana wenyewe,” alisema Zitto.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Taasisi isiyokuwa ya kiserikali ya Twaweza, Rakesh Rajani alisema vijana wanapaswa kuyapa kipaumbele masuala yanayohusu elimu kwa sababu huo ndiyo urithi usiohamishika.

“Elimu ndiyo kila kitu. Mnapojadili katiba angalieni mambo ambayo mnaweza kuyaweka katika Katiba Mpya,” alisema Rajani.

Meneja Uhusiano wa Femina HIP, Lilian Nsemwa alisema lengo la kuandaa kongamano hilo ni kuwawezesha vijana kutumia haki yao ya kushiriki katika mchakato wa kupata Katiba Mpya.

No comments:

Post a Comment