Saturday, April 7, 2012

Rais Kikwete atangaza wajumbe wa tume ya katiba





 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 
 RAIS Jakaya Kikwete amemteua Waziri Mkuu Mstaafu, Joseph Warioba kuwa Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya Katiba Tanzania. Pia amemteua na Jaji Mkuu Mstaafu, Augustino Ramadhani kuwa makamu wake.

Akitangaza Tume hiyo Ikulu, Dar es Salaam jana, Rais Kikwete alisema Tume hiyo itasaidiwa na Sekretarieti itakayoogozwa na Katibu Mtendaji, Asaa Ahmad Rashid na Naibu wake ni Casmir Sumba Kyuki.

Hii ni mara ya pili kwa Warioba, Mwanasheria Mkuu wa zamani wa Serikali ambaye pia aliwahi kuwa Jaji katika Mahakama ya Kimataifa ya Mazingira kupewa jukumu la kusimamia tume zinazovuta hisia za mamilioni ya Watanzania kwani ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya Kuondoa Kero ya Rushwa nchini iliyoundwa na Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamin Mkapa.

Jaji Ramadhani kwa upande wake, mbali ya kuwa Jaji Mkuu wa Tanzania kwa miaka sita, wadhifa aliokuwa nao hadi alipostaafu Desemba 27, 2010 na nafasi yake yake kuchukuliwa na Jaji Mkuu wa sasa, Mohamed Chande Othman alikuwa, Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) na baadaye Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC) kwa wadhifa huo huo. Pia alikuwa Brigedia Jenerali wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), hadi alipostaafu mwaka 1997.

Kwa upande wa Asaa kabla ya uteuzi huo alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Sheria Zanzibar wakati Kyuki alikuwa Mwandishi Mkuu wa Sheria katika Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Tanzania Bara.

Rais Kikwete aliwaambia wahariri na waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari kwamba uteuzi wa Tume hiyo ni hatua ya kwanza muhimu katika mchakato wa kuiwezesha nchi kupata Katiba Mpya ifikapo mwaka 2014.

“Sheria yetu inaelekeza Tume hii iwe imekamilisha kazi yake ndani ya miezi 18, sasa kama wakianza kazi tuseme Mei watakuwa na miezi minane mwaka huu na kwa maana hiyo mwakani inabidi wamalize kazi hiyo Oktoba, miezi 18 itakuwa imekamilika,”alisema Rais Kikwete na kuongeza:

“Sasa kama ni hivyo mimi sioni kwa nini ifikapo mwaka 2014 tusiwe na Katiba Mpya… hili linawezekana kabisa.”
Wajumbe wengine
Tume hiyo ina uwakilishi wa makundi mbalimbali katika jamii. Yumo mwanadiplomasia wa siku nyingi Waziri Mkuu Mstaafu na Katibu Mkuu wa uliokuwa Umoja wa Nchi Huru za Afrika (OAU), Dk Salim Ahmed Salim, Mshauri wa  wa Chadema, Profesa Mwesiga Baregu na Mkuu wa Idara ya Sheria, Katiba na Haki za Binadamu wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Dk Sengondo Mvungi.

Tume hiyo ambayo inaundwa na wajumbe 30 nusu kutoka kila upande wa Muungano, pia inawajumuisha aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Said El Maamry, Mbunge wa Viti Maalumu, Al-Shaymaa Kwegyir, Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku na Mhadhiri mwandamizi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Profesa Palamagamba Kabudi.

Rais Kikwete aliwataja wajumbe wengine wa Tume hiyo kutoka Tanzania Bara kuwa ni Katibu Mkuu wa Chama cha Walimu Tanzania (CWT), Yahya Msulwa, Mwenyekiti wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF), Esther Mkwizu, Riziki Mngwali, Richard Lyimo, John Nkolo, Jesca Mkuchu, Humphrey Polepole, Maria Kashonda na Mwantumu Malale.

Wajumbe kutoka Zanzibar ni wamo Mwandishi wa habari mkongwe, Ally Salehe, Fatma Said Ali, Omar Sheha Mussa, Raya Salim Hamadi, Awadh Ali Said, Ussi Khamis Haji, Salma Maoulidi, Nassor Khamis Mohammed, Simai Mohammed Mshamba, Kibibi Mwinyi Hassan, Suleiman Omar Ali, Salama Kombo Ahmed na Abubakar Mohammed Ali.

Rais Kikwete alisema mchakato wa uteuzi wa wajumbe hao ulizingatia matakwa ya kisheria yanayomwelekeza kushauriana na Rais wa Zanzibar.

Alisema kabla ya kuteua majina hayo, walipokea mapendekezo ya majina zaidi ya 550 kutoka kwa wadau mbalimbali akisema ilikuwa kazi ngumu kuyachuja na kubaki na majina hayo kama sheria inavyoelekeza.

“Tumejitahidi kadri ya uwezo wetu maana kama si haya mapendekezo pengine tungeishia kuteua wale tunaowafahamu tu, lakini tumejitahidi kugusa kila kundi. Tunafahamu kwamba hatuwezi kumridhisha kila mtu, lakini wale ambao hawakupata nafasi katika Tume basi watatumia fursa nyingine ambazo zipo kupitia mchakato huu,” alisema Rais Kikwete.

Muda wa Tume
Rais Kikwete alisema wajumbe wa Tume hiyo wataapishwa wakati wowote kuanzia sasa ili kuwawezesha kuanza safari yao ya miezi 18 ya kukusanya maoni ya wananchi kuhusu Katiba Mpya na kukamilisha kuandikwa kwa Katiba hiyo.
Rais alisema Tume hiyo baada ya kukamilisha kazi yake ya kukusanya maoni ya Watanzania na kutengeneza rasimu ya Katiba, zitakuwa zimebaki hatua mbili muhimu ambazo ni kuundwa kwa Bunge maalumu na kura ya maoni.

“Baada ya hatua hiyo kukamilika, rasimu itawasilishwa katika Bunge maalumu ambalo litaundwa kwa ajili ya kujadili na kuchambua mambo yanayofaa yaliyomo katika rasimu hiyo, Bunge hili litakuwa kwa ajili hiyo tu na likishakamilisha kazi yake basi muda wake utakuwa umeisha” alisema Rais Kikwete.

Alisema baada ya mambo ya msingi kupitishwa na Bunge hilo, mchakato huo utarejeshwa kwa wananchi ambao watapiga kura za maoni kama wataona yaliyopitishwa yanafaa au la.

Rais ametangaza kuundwa kwa Tume hiyo siku chache tangu yafanyike mabadiliko katika Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, katika Mkutano wa Sita wa Bunge la 10, marekebisho ambayo yalizua manung’uniko kutoka kwa wabunge wa CCM.

Katika hotuba yake ya Desemba 31, 2010, Rais Kikwete aliahidi kuanzisha mchakato wa kuandikwa kwa Katiba mpya ambayo alisema italivusha Taifa katika miaka mingine 50 ikiimarisha udugu na mshikamano wa Watanzania.

Wateule wanena

Wakizungumza kwa nyakati tofauti, baadhi yawajumbe walioteuliwa katika Tume hiyo walisema kuwa ni mapema mno kuzungumzia uteuzi wao.

Dk Mvungi alisema kazi hiyo ni kubwa kwa kuwa wanaotumikiwa ni wananchi, huku akiomba kupewa muda hadi leo ili aweze kutafakari cha kuzungumza.

“Muda mfupi uliopita ndiyo nilipata taarifa ya uteuzi huo ila nahitaji kujishauri kwanza pia kusikiliza ushauri wa familia yangu, naomba unipe muda hadi kesho (leo), naweza kuwa na cha kuzungumza zaidi,” alisema Dk Mvungi.

Kwa upande wake Butiku alisema mpaka alipokuwa akipigiwa simu kuulizwa alivyopokea uteuzi wake alikuwa hajapata taarifa za uteuzi huo. Alisema atazungumza mara baada ya kuthibitisha rasmi kuwa ameteuliwa.

“Hivi tunavyozungumza ndiyo nafika Musoma nikitokea Mwanza, sijapata taarifa yoyote, ngoja kwanza nisubiri taarifa rasmi ili niweze kuzungumza vizuri.”

No comments:

Post a Comment